Header Ads

ad

Morata utaiweza jezi No. 9? Wenzako walipotea Chelsea wakiwa na jezi hii

Na Salym Juma, Arusha
Alvaro Morata ni mshambuliaji hatari ambaye amefanya makubwa Juventus na Real Madrid kiasi ambacho Chelsea wameshawishika kutoa £60m kumsajili mchezaji huyukutoka Madrid. Ubora wake ulimfanya awindwe na Manchester United pia. Japokuwa alikuwa anatokea benchi, Morata aliweza kufunga magoli 20 msimu uliopita akiwa Madrid baada ya kurejea kutoka Juve. Baada ya kumwaga wino Chelsea, Morata alikabidhiwa jezi namba 9.
Jezi hii imeonekana sio lolote siku za karibuni katika klabu ya Chelsea kwani Hernan Crespo ndiye mchezaji pekee ambaye kumbukumbu zangu zinaonesha ‘atleast’ aliitendea haki jezi hii tofauti na wengine. Uwezo wa Morata ni mkubwa kwani ana uzoefu wa ligi kubwa mbili, La liga na Serie A. Morata pia ana uzoefu wa Michuano ya Ulaya ila jezi namba 9 haina upepo mzuri pale Cobhan na Darajani. Leo hii tujaribu kuwatazama baadhi ya wachezaji ambao hawakufanya vizuri pindi walipopewa jezi hii.
Wachezaji hawa walionekana wazuri kwenye Vilabu vyao ila baada ya kwenda Chelsea na kuvaa namba 9 mgongoni hali ilikuwa tete….
Fernando Torres, £50 million ndio zilimng’oa Anfield mnamo January 31, 2011 na kuufanya uhamisho wake kuvunja rekodi pale Uingereza. Torres alisajiliwa kwa mbwembwe za aina yake hasa kutokana na kiwango chake bora alichokionesha akiwa Liverpool. Wiki Moja baadae Torres alianza kuichezea Chelsea dhidi ya timu yake ya zamani ya Liverpool. Baada ya kupewa jezi namba 9, namba ambayo ndiyo iliyompa mafanikio Anfield, Torres alishindwa kabisa kung’ara Darajani.
Dunia ilikuwa inasubiri kuona ni lini Torres atafunga hali ambayo ilimpa presha kubwa mshambuliaji huyu ambaye atakumbukwa na Chelsea kwenye mechi ya nusu fainali ya UEFA dhidi ya Fc Barcelona. Baada ya dakika 903 sawa na Mechi 14, hatimaye Torres aliweza kufunga goli lake la kwanzaakiwa Chelsea pale ambapo waliilaza 3-0 West Ham. Kazi nzuri ya Frank Lampard na Florent Malouda ilimfanya Toress kumaliza ukame. Hadi anaondoka Chelsea alifunga magoli 45 katika michezo 172.
Radamel Falcao ni jembe lingine ambalo lilifanya vizuri sana Hispania na Ureno kwa nyakati tofauti. Uwezo wake wa kufunga ulimfanya asajiliwe Monaco kabla ya kwenda Man United na baadae Chelsea ambapo alikabidhiwa jezi namba 9. Japo alishajifia Man United ila upepo mbaya wa jezi hii kunako Chelsea katika miaka ya kaaribuni ulimfanya Falcao azidi kupotea katika kupasia kamba. ‘The Tiger’ kama anavyohamika pale Madrid alishindwa kabisa kung’ara na jezi hii.
Ikumbukwe July 3, 2015 Falcao alisajiliwa Chelsea kwa mkopo huku kukiwa na kipengele cha kumbakiza moja kwa moja Darajani endapo angefanya vizuri pale London. Kama ilivyokuwa kwa Torres, Falcao nae alikuwa anasubiriwa lini atafunga goli na presha ilikuwa kubwa sana upande wake. Ilimchukua hadi 29 August pale alipofunga goli la kusawazisha dhidi ya Crystal Palace pale Blues walivyolazwa nyumbani. Hadi anaondoka pamoja na majeraha Falcao alikuwa amefunga goli 1 katika mechi 12.
Mateja Kežman baada ya kufanya vyema PSV kwa kufunga magoli 105 katika 122 hatimaye Chelsea ya José Mourinho ilimsajili mshambuliaji huyu mtukutu. Kiwango chake cha kuridhisha kilimfanya mmiliki wa Chelsea asiwe bahili kutoa pesa hasa katika kipindi hiki ambacho walikuwa wanafanya mapinduzi ya kikosi. Kezman alikabidhiwa jezi namba 9 ambayo iliendelea kuwa na upepo mbaya kwa wachezaji wa Chelsea wanaosajiliwa katika idara ya ushambuliaji.
July 13, 2004 Chelsea ilitoa kiasi cha £5.3 million na kunasa saini ya Mserbia huyu ambaye alikwenda kufanya vibaya Darajani akiwa na jezi namba 9. Akiwa Chelsea Kezman hakufanya vizuri kwani katika michezo 41 alifunga mara 7 tuu.  Mimi ni miongoni mwa watu wengi ambao tuliamini Chelsea imepata dodo chini ya mnazi kwani Kezman alikuwa na kila ubora ambao unaujua wewe katika kupasia Kamba ila mwisho wa siku mambo yakawa tofauti.
Khalid Boulahrouz ni beki kutoka Uholanzi ambaye alisajiliwa na Jose Mourinho pale Cobhan. Japokuwa hakuwa mshambuliaji kama wenzake kwenye listi hii ila nae hakufanya vyema Darajani kama ilivyokuwa kwa Hamburger SV na RKC Waalwijk. Khalid alikabidhiwa jezi namba 9 ambayo ilivaliwa na Muargentina Hernan Crespo ambaye ‘at-least’ aliitendea vyema Jezi hii ambayo imekuwa na upepo mbaya pale Darajani hasa katika miaka ya karibuni.
Steve Sidwell ni mchezaji mwingine ambaye anakamilisha listi hii fupi ya wachezaji wa Chelsea ambao wamefanya vibaya wakiwa na jezi namba 9 mgongoni. Akiwa Reading, Sidwell alifanya makubwa hadi kufikia hatua Chelsea kumsajili kabla ya kufanya vibaya kwa kuondoka bila kufunga hata goli moja katika michezo 15 aliyopata nafasi pale Darajani. Baada ya kuondoka Chelsea, Sidwell alishindwa kung’ara hata huko alipoelekea na hali hii inamkumba hadi sasa kule Brighton & Hove Albion.