Header Ads

ad

Starehe za Neymar huenda zikampeleka Dybala Camp Nou

Na Salym Juma, Arusha
Brazil ni nchi inayopatikana Kusini mwa Amerika. Nchi hii imejaaliwa watu wenye Vipaji lukuki hasa mpira wa miguu. Brazil imejaaliwa warembo wazuri ambao wamekuwa wakipamba miji mbalimbali kwa urembo wao. Ipo siku nitakuja na makala inayoelezea starehe kwa ujumla nchini Brazil. Wanasoka wengi wa Brazil wamekuwa mstari wa mbele katika suala la starehe kama ilivyo jadi ya nchi yao. Kumbuka hata viongozi wa siasa wa Brazil wamewahi kukumbwa na kashfa ya wizi kisa starehe.
Wapo wachezaji kibao wa Brazil ambao muda mfupi baada ya kustaafu wameonekana kwenye starehe huku wengine miili ikituna na hii ni ishara ya kutofanya mazoezi licha ya kustaafu. Ronaldinho alikuwa ni nyota aliyeiteka Dunia ila starehe za hapa na pale zilichagiza Barcelona kumuuza licha ya kuwa tegemeo lao kwa wakati huo. Wabrazil wamekuwa wakiamini starehe zilizopitiliza ni jambo ambalo halipingiki inawezekana ni kwasababu wengi walikuwa na ndoto hizo za ‘matanuzi.’
Neymar ni mchezaji tegemeo wa Brazil na amekuwa pia akiisaidia Barcelona kwa misimu kadhaa sasa. Mshambuliaji huyu kwa wiki kadhaa amekuwa akipiga Picha nyingi sehemu za starehe tofauti na wachezaji wengine. wakati ligi ikiwa inaendelea alionekana akiwa anakula ‘Bata’ viwanjani kama kawaida. Neymar alianza ‘ku-trend’ kwenye masuala ya starehe tangu akiwa nchini kwao kabla ya kuhamia Ulaya, sehemu ambayo imezidi kumpa umaarufu.
Baada ya Barcelona kuitoa PSG kwenye robo fainali ya UEFA, usiku wake Neymar alienda kufanya ‘matanuzi’ na muendesha magari ya langalanga Lewis Hamilton, baada ya kutoka kwenye ‘matanuzi’ siku iliyofuata aliumia kwenye mazoezi na kukosa mchezo uliofuata wa ligi dhidi ya Deportivo ambapo Barca walipoteza. Inawezekana starehe ndiyo ilisababisha yote haya. Tetesi za uhamisho wa Neymar kwenda PSG huenda zikawa kweli kutokana na Barca kuanza kuchoshwa na starehe hizi.
Paulo Dybala ni mchezaji hatari wa Juventus anayekipiga timu ya taifa ya Argentina. Mara kadhaa Dybala na Neymar wamekuwa wakitajwa kuwa Messi na CR7 wa baadae. Ni wazi kuwa matajiri wa PSG wapo radhi kuvunja Benki na kumsajili Neymar ambaye ameanza kuonesha dalili za kuondoka Barcelona. Dybala ndie anaetajwa mara nyingi kurithi nafasi ya Neymar. Tetesi za kusajiliwa kwake zilianza mapema sana kabla PSG hawajafikiria kutangaza kumtaka Neymar.
Paulo Dybala ana uwezo mkubwa sana wa kulazimisha, kupiga chenga za maudhi na kufunga pia. Kiukweli binafsi nimekuwa mwepesi kuamini Neymar, Hazard na Dybala watakuja kurithi nafasi za Messi na CR7 baada ya miaka miwili au zaidi. Paulo Dybala ana kila sifa ya kurithi nafasi ya Neymar muda wowote PSG wakimuweka chini ya mikono yao. Kwa misimu miwili aliyocheza Juve katika michezo 94 ameweza kufunga mara 42. Uwezo wake uwanjani Barca wanaujua vizuri.
Japokuwa mwezi April, Dybala alisaini mkataba wa miaka 5 wenye thamani ya €7million kwa mwaka utakaomuweka Juve hadi June 2022 ila bado haiwanyimi Cataluna kufanya yao pindi wakiwa ‘serious’ hasa endapo Neymar ataondoka. Mpaka sasa Juve haijapata ‘Pesa ndefu’ kwenye usajili hasa baada ya kuwabania Chelsea kuhusu Sandro. Nina mashaka na Juve kwani inawezekana wanataka kufanya ‘dili takatifu’ la kulala maskini na kuamka tajiri dakika za mwisho.
"I'm not afraid to lose Dybala" hii ni kauli aliyosema Massimiliano Allegri siku za karibuni baada ya tetesi za Dybala kwenda Barca kutanda. Ukijaribu kuichimba kauli hii unaweza kugundua Juve wameanza kujiandaa kisaikolojia kumkosa Dybala. Juve wana rekodi ya kuuza wachezaji tegemeo bila kujali na bado wamekuwa wakifanya vyema Italia na barani Ulaya. Dybala ni mchezaji mdogo kiumri na mwenye kiwango murua hivyo atafanya vyema Barca.
"I do not know firsthand what's happening with Neymar and PSG, so I do not know if that premise will be fulfilled if Barcelona has to sign a substitute. I'm not worried," hii ni kauli nyingine ya Allegri siku ya Ijumaa alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari. Barcelona watapambana kutafuta saini ya Paulo endapo Neymar ataondoka.  Zaidi ya Dybala, kwa sasa hakuna mchezaji sokoni ambaye Barca wanaweza kumsajili kuziba pengo la Neymar kama waarabu wakiwa tayari kulipa €222million.